Mauaji ya kutisha yametikisha wilaya ya Tarime kiasi cha kumfanya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kutuma timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi hilo inayohusisha kamisheni ya Operesheni kufanya uchunguzi.
Hatua ya kupelekwa kwa timu hiyo inatokana na mauaji ya mfululizo katika
mji wa Tarime ambayo ipo kwenye himaya ya Kanda Maalum ya Polisi ya
Tarime na Rorya ambayo yametokea kwa watu wanane katika kipindi cha siku
tatu.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na jambazi mwenye silaha katika mji wa
Tarime mkoani Mara kwa siku tatu kuanzia Jumatatu hadi jana.
Mmoja wa watu waliouawa ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Koplo Zakaria Chacha Mwita ambaye ni mtoto wa marehemu
Meja Jenerali Mwita Marwa.
Pia wamo aliyekuwa Mhandisi Ujenzi Wilaya ya Rorya, aliyetajwa kwa jina la David Mwasi Misiwa.
Wengine ni mfanyabiashara, Samuel Richard Mohenga na huku Jeshi la Polisi likisema kuwa linaendesha msako.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Royra, Justus Kamugisha,
alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa mtu anayesadikiwa
kuwa jambazi akiwa na bunduki kwa siku tatu kuanzia Januari 26, mwaka
huu usiku aliua watu saba kwa kuwapiga risasi na kujeruhi kadhaa.
Aliwataja wengine kuwa ni mwendesha bodaboda, mkazi wa kijiji cha
Nkende, Juma Marwa Nyaitara, Erick Lucas Makanya, mfanyabiashara wa
bucha mkazi wa kijiji cha Rebu, Juma Mwita Mroni na mkazi wa kijiji cha
Kenyamanyori, Robert Chacha Kisiri.
Jana asubuhi, wakazi wa mji wa Tarime na vitongoji vyake walimfananisha
mtu aliyekuwa amevaa koti refu na mtuhumiwa wa mauaji hayo na kutaka
kumshushia kipigo, lakini aliokolewa na polisi waliorusha risasi hewani
na kumpeleka katika kituo cha polisi.
Kamanda Kamugisha aliwashauri wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mara watakapomuona mtuhumiwa.
Alisema polisi wanafanya msako katika vijiji vya Kenyamanyori, Rebu,
Nkende, Mogabiri na Kibumaye katika kata za Kitare, Turwa na Binagi
kwenye Tarafa ya Inchage.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John
Henjewele wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya
Tarime jana walitembelea maeneo ya vijiji ambavyo wakazi wake wameuawa
na jambazi hilo.
TIMU YA MAKAO MAKUU
Alizungumzia timu iliyotumwa Tarime, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa
Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, alisema kuwa ni ya
wapelelezi na Intelijensia na inakwenda kuongeza nguvu katika juhudi
zinazofanywa na mkoa wa Mara kuhakikisha jambazi huyo anakamatwa ili
kuondoa hofu kwa wananchi.
Chagonja alisema juhudi za kumsaka jambazi huyo zinaendelea kufanywa na
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja
na wananchi.
SOPHIA SIMBA ALAANI MAUAJI
Wakati huo huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia
Simba, amelaani maauji ya wanawake watano waliotaarifiwa kuuawa katika
wilaya za Musoma, Butiama na Rorya mkoani Mara.
Alisema wizara inasisitiza kuwa mtazamo huo ni hasi na unakwenda kinyume
cha haki za binadamu hivyo jamii haina budi kuachana na imani
zinazosababisha mauaji.
“Wizara inahimiza wananchi kupinga dhana potofu zinazopelekea mauaji
ya wanawake ikiwa ni pamoja na imani za kishirikina, uchu wa kupata
utajiri wa haraka, kulipiza kisasi na kuendeleza hulka ya ukatili katika
jamii,” alisema.
Alisema: “Mauaji dhidi ya wanawake yanapotokea katika jamii zetu
yanarudisha nyuma juhudi za serikali katika kuzuia ukatili dhidi ya
wanawake katika jamii kutokana tu na tofauti za kimaumbile.
Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya kuthaminiwa
utu wao na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao
unaweza kuhatarisha haki yao ya kuishi ambayo ndiyo haki kuu kuliko haki
zote,” alisema na kuongeza:
“Kushamiri kwa mauaji ya kikatili wanayofanyiwa wanawake katika wilaya
za mkoa wa Mara ni jambo ambalo linasababisha hofu kubwa miongoni mwa
wanawake. Mauaji hayo yanawakosesha amani na utulivu na hivyo
kuzorotesha ari yao katika shughuli za uzalishaji mali.”
CHANZO:
NIPASHE