Home »
» "CHADEMA NI CHAMA CHA WAHUNI" ASEMA MWIGAMBA... Asema kitavuruga ndoto za Watanzania Afichua ya Zitto Kabwe na chama kipya
"CHADEMA NI CHAMA CHA WAHUNI" ASEMA MWIGAMBA... Asema kitavuruga ndoto za Watanzania Afichua ya Zitto Kabwe na chama kipya
Posted by Unknown
Posted on Wednesday, March 05, 2014
WAKATI maandalizi yote ya uzinduzi wa chama kipya cha ACT-Tanzania yakiwa yamekamilika, Katibu Mkuu wake Samson Mwigamba, ameiponda CHADEMA kuwa ni kusanyiko la wahuni na si wanasiasa.
Amewatahadharisha Watanzania kutokubali kurubuniwa na kauli kuwa CHADEMA ndio mkombozi wa taifa.
Amesema viongozi wa chama hicho asilimia kubwa wapo kwa ajili ya maslahi binafsi.
“Watanzania wawangalie na ikibidi wawapuuze, nilikuwepo nafahamu kila kinachoendelea, pale hakuna chama licha ya kujinadi kuwa wakombozi wa wananchi, ni waongo wakubwa.
“Kuna watu wapo pale kwa ajili ya maslahi binafsi na familia zao, hakuna mtanzania atakayetetewa wala kuletewa maisha bora kama watakiweka madarakani,’’ alisema Mwigamba katika mahojiano na gazeti hili jana.
Alisema CHADEMA inatumia mabavu na kuchochea vurugu kwa kuwa hakuna kiongozi bora mwenye uwezo wa kuwaongoza wananchi zaidi ya kusheheni viongozi wa matukio na si wa kuwazungumzia wananchi.
Mwigamba alisema kupitia chama chao, wamejipanga kuleta mabadiliko ya kisiasa hasa kwa vyama vya upinzani nchini, ambapo alisema muda wowote kuanzia leo, wanatarajia kupewa usajili wa kudumu wa chama hicho.
Alisema hawajakianzisha chama hicho ili kuhujumu upinzani, bali kukidhi haja ya watanzania.
Alikanusha uvumi kuwa wanatumiwa na CCM kuvuruga upinzani nchini.
Alisema hayo ni mawazo ya watu wasio na ufahamu mzuri.
“Tulikuwa na mipango ya kwenda mkoani Mwanza kufanya mkutano wa hadhara, tumeshindwa baada ya kukosa fedha, ila tutafika kwa nguvu zetu wenyewe mkoani humo na mikoa mingine nchini,” alisema Mwigamba.
Akizungumzia madai ya chama hicho kufadhiliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, Mwigamba alisema si za kweli.
“Hatufadhiliwi na Zitto na tutasimama kwa nguvu yetu, japokuwa tunamuhitaji na tumeanza naye mazungumzo ili kumuomba ashirikiane nasi katika harakati za kuleta mabadiliko,” alisema Mwigamba.
Alisema bado hawajafanikiwa kumshawishi Zitto, licha ya kuwa wamejipanga kuwa na wanasiasa makini wenye mtazamo wa mabadiliko.
“Sheria haziruhusu Zitto kuwa na vyama viwili, yeye ni mwanachama halali wa CHADEMA kwa kuwa ana kesi mahakamani. Kama akipenda kuja aje na asifikirie ubunge wake kwani tunamuhitaji,” alisema.
Pia, alisema mbali ya kumshawishi Zitto kujiunga na Chama hicho, walikuwa na mpango wa kumshawishi Dk. Kittila Mkumbo ajiunge na chama hicho, wamekwama.
Alisema Dk. Kittila aliwaambia hataki tena kujihusisha na masuala ya siasa.
Mwigamba na Mkumbo walifukuzwa CHADEMA kwa madai ya kuandaa waraka wa siri waliouita wa mabadiliko ya uongozi uliokuwa ukieleza harakati za kuwang’oa viongozi walioota mizizi.
MATUKIO YA VURUGU YA CHADEMA
Viongozi na wafuasi wa chama hicho wanatuhumiwa kushiriki kwenye matukio ya vurugu ambazo baadhi zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania.
Vurugu nyingi hutokea kwenye mikutano ya hadhara hasa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Kwa sasa wanadaiwa kupeleka makundi ya vijana kutoka mikoa mbalimbali katika jimbo la Kalanga mkoani Iringa, ambako kunatarajia kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge.
Inadaiwa chama kiliingiza silaha mbalimbali jimboni humo vikiwemo visu, mapanga na marungu, ambazo zimekamatwa.