Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fahmi Dovutwa alichafua hali ya hewa baada ya kuvituhumu vyama vya CCM, Chadema na CUF kuwa ndiyo vinavuruga Bunge kwa sababu ya misimamo yao.
Hali hiyo ilitokea wakati mjumbe huyo akichangia mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba juzi.
Dovutwa alitoa shutuma hizo baada ya mjumbe
mwingine, Julius Mtatiro kueleza kuwa amepitia Rasimu ya Kanuni lakini
hakuona mahali panapoeleza mpangilio wa ukaaji wakati wa kupiga kura.
Hali hiyo ilimfanya Dovutwa, kusimama na kutoa
tuhuma kuwa baadhi ya wajumbe wamehongwa na kwamba kuruhusu mpangilio
maalumu ni kukaribisha mgawanyiko.
Alisema kukaa kwa mpangilio huo kutawapa nafasi viongozi mbalimbali kushinikiza wajumbe wao katika maamuzi ya mambo mbalimbali.
“Ukaaji wa sasa umezingatia masilahi ya nchi,
utashi na matakwa ya wananchi. Watu wa CCM, CUF na Chadema ndiyo
mnaharibu mkutano (Bunge),” alisema Dovutwa.
Dovutwa alisema vyama hivyo vinatofautiana katika masuala mbalimbali na misimamo yao ndiyo imetawala bunge hilo.
“Mnatulazimisha tuwasikilize nyie tu. Kwa hiyo
Mwenyekiti usikubali, kikao hiki kizingatie masilahi mapana ya makundi
mbalimbali,” aliongeza Dovutwa.
Baada ya kutamka hilo, mmoja wa wajumbe wa Kamati
ya Kupitia Kanuni, Amon Mpanju alisimama na kumtaka Kificho kulisaidia
Bunge hilo kwenda na utaratibu aliowatangazia juzi wajumbe, ambao
wanatakiwa kuwasilisha hoja zao kwenye kamati kisha kutolewa uamuzi.
“Naomba uamuzi ukishafanyika, kiti chako
kisiruhusu mtu mwingine kuingilia maana mchakato hautafika mwisho.
Nawaomba wajumbe wenzangu tusilete michango inayoweza kuleta hisia za
mgawanyiko miongoni mwetu,” alisema Mpanju.
Mtatiro alisema hakupendezwa na mchango wa Dovutwa
na kutahadharisha ukweli hauwezi kukwepeka kwa kuwa kuna watu wanaotoka
katika makundi mbalimbali.
“Wakati wa kupiga kura tunahitaji theluthi mbili
ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo kwa wajumbe kutoka
Zanzibar kwa hiyo ili kurahisisha kazi hiyo, wajumbe kutoka Zanzibar
wakae upande wao na wale wa Bara wakae upande wao,” alisema Mtatiro.
-mwananchi
-mwananchi