WATU tisa akiwemo Diwani wa Kata ya Old Moshi
Magharibi, Elisaria Mosha (Chadema) wametiwa mbaroni wakituhumiwa kupokea fedha
kwa njia ya udanganyifu kupitia mradi wa umeme mkoani Kilimanjaro.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Makamu wa Rais Dk
Mohamed Gharib Bilal, kufanya ziara mkoani Kilimanjaro na kuagiza watu
waliofanya hivyo wakamatwe mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema diwani huyo
anatuhumiwa kujipatia Sh milioni 9.6 kwa njia ya udanganyifu.
Wengine wanaoshikiliwa ni Zakayo Kimathi (52) mkazi wa
Mandaka, anayedaiwa kupokea Sh milioni 10.3, Oforo Kimambo (56) mkazi wa
Mandaka anayedaiwa kupokea Sh milioni 29.
Wengine wanaotuhumiwa kupokea malipo hayo kwa njia ya udanganyifu
ni Daud Mallya (69) mkazi wa Chekereni aliyepokea Sh milioni 8.6, Richard Mlaki
(69) mkazi wa Kiboroloni alipokea Sh milioni 18.6 na Focus Herman (88) mkazi wa
Kilototoni aliyepokea Sh milioni 36.
Boaz alisema kwa sasa watuhumiwa watatu hawajapatikana.
Alieleza kuwa pamoja na watuhumiwa hao, polisi imemkamata Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mandaka Monono, Hassan Nduva (41) na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho,
Vendelini Shayo (58) kwa kuhusika kufanikisha malipo hayo.
Dk Bilal alitoa agizo hilo mapema wiki hii wakati
akizindua vituo vya kupozea na kusambaza umeme maeneo ya Kiyungi, YMCA na
Makuyuni.
Alipokea taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kuwapo kwa wananchi
ambao hawakulipwa fidia zao, kutokana na kuwapo watu waliotumia ujanja wa
kupokea fedha hizo, Sh milioni 169.2.
“Halmashauri ya Moshi Vijijini ndio ilikuwa wakala wa
malipo hayo na ndio iliyofanya tathmini kwa kushirikiana na watendaji wa
vijiji, ambapo wao walipeleka tathmini hiyo kwa Shirika la Umeme (Tanesco),
ambalo lilitoa fedha hizo hivyo Tanesco hawahusiki,” alisema,” alisema Boaz.
-Habarileo