·
TAASISI ya Mwalimu Nyerere Foundation kwa kushirikiana na Kampuni ya
Push Mobile, imezindua teknolojia ya kuwezesha Watanzania kusikiliza na
kuangalia hotuba za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia simu
za mkononi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Joseph Butiku alisema wameamua
kuanzisha mpango huo, kuwawezesha Watanzania, Waafrika na dunia kujua kazi
alizozifanya marehemu Baba wa Taifa kwa jamii.
Butiku alisema ili kupata hotuba hizo kupitia simu ya mkononi, unatakiwa
kutuma neno Hotuba kwenda namba 15678 .
Vile vile, unaweza kupata picha nyingi zaidi kwa kuingia
www.simu.tv/nyerere mobile tv. Alisema mpango huo upo kwa njia ya CD na DVD,
ambazo Watanzania wengi wameanza kuzichangamkia kupata nakala.
“Huu ni mpango maalumu wa kuhakikisha kumbukumbu za marehemu Baba wa
Taifa zinapatikana kiganjani na muda wowote, tumeingia makubaliano maalumu na
Kampuni ya Push Media Mobile ili kuendeleza juhudi hizi za kuenzi enzi zake,”
alisema Butiku.
Alisema Mwalimu amefanya kazi kubwa za kuelimisha kwa kutunga vitabu
mbalimbali, ambavyo vingi vimekuwa vikutumika kusaidia mambo mbalimbali ya
kisiasa na uchumi.
“Nakumbuka alisema kuwa mawazo haya yapo kwenye vitabu na kanda
mbalimbali, yatumike katika kuchangia maendeleo ya binadamu, alikuwa mwangalifu
sana kwani yamezingatia hali halisi ya jana na leo, natoa ushauri kwa
Watanzania kutumia mpango huu ili kusaidia Taifa,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Push Mobile Media, Freddie Manento alisema
wameingia makubaliano na Taasisi ya Mwalimu Nyerere lengo kubwa ni kurahisisha
kupatikana busara za Mwalimu kwa Watanzania wote, ikiwa pamoja na vizazi vya
sasa.
-Habarileo