MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne, umeingia dosari baada ya walimu wawili akiwamo Mkuu wa Shule, wamekushikwa wakishiriki kutoa majibu kwa wanafunzi wao.
Tayari
Polisi mkoani Singida, inashikilia walimu hao wa Sekondari ya Nkinto
wilayani Mkalama kwa tuhuma ya kuvujisha mtihani huo unaoendelea
kufanyika nchini kote hivi sasa.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alitaja watuhumiwa hao
kuwa ni Mkuu wa Shule, Monica Sebastian (30) na msimamizi wa mtihani
huo, Agaloslo Otieno (32).
Alisema
watuhumiwa hao walivujisha mtihani huo juzi kati ya saa 3 na 3:30
asubuhi katika shule hiyo iliyopo Kata ya Mwangeza Tarafa ya Kirumi.
Alidai
kuwa Mwalimu Agaloslo aliyekuwa akisimamia mtihani katika shule
nyingine ya Mwangeza, aliandika baadhi ya maswali ya Kiswahili na Uraia
kwenye simu yake ya mkononi na kumtumia Mkuu wa Shule yake ya Nkinto,
Monica aliyekuwa shuleni kwake.
Baada
ya Monica kupata maswali hayo, inadaiwa alitafuta majibu akiwa chooni
huku wanafunzi wakimfuata huko huko na kupewa majibu.
Kamanda
Kamwela alisema lengo lao lilikuwa kusaidia wanafunzi, wafanye vizuri
katika mtihani wao wa kidato cha nne mwaka huu. Alisema wanafunzi
waliishaambiwa wadanganye wanakwenda chooni, ili wakapewe majibu na Mkuu
wa Shule.
"Uchunguzi
wa awali unaonesha kuwa uvujishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti
kati ya Monica na Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika
shule tofauti.
“Baada
ya Mkuu wa Shule kutumiwa maswali, alijificha chooni na watahiniwa kwa
nyakati tofauti waliomba ruhusa kwa wasimamizi kwenda kujisaidia na hapo
walimkuta Mkuu wa Shule na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali
hayo," alisema Kamanda Kamwela.
Alisema
baada ya Polisi kupata taarifa ya siri kutoka kwa wasamaria, iliweka
mtego katika Sekondari ya Nkinto na kumkamata Mwalimu Monica huku simu
yake ikiwa na baadhi ya maswali ya mtihani.
-Habari Leo
-Habari Leo