muhtasari

Latest Article Get our latest posts by subscribing this site

MTIHANI KIDATO CHA NNE 2013 WAINGIA DOSARI BAADA YA KUVUJA...



MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne, umeingia dosari baada ya walimu wawili akiwamo Mkuu wa Shule, wamekushikwa wakishiriki kutoa majibu kwa wanafunzi wao.
Tayari Polisi mkoani Singida, inashikilia walimu hao wa Sekondari ya Nkinto wilayani Mkalama kwa tuhuma ya kuvujisha mtihani huo unaoendelea kufanyika nchini kote hivi sasa.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu wa Shule, Monica Sebastian (30) na msimamizi wa mtihani huo, Agaloslo Otieno (32).
 
Alisema watuhumiwa hao walivujisha mtihani huo juzi kati ya saa 3 na 3:30 asubuhi katika shule hiyo iliyopo Kata ya Mwangeza Tarafa ya Kirumi.
 
Alidai kuwa Mwalimu Agaloslo aliyekuwa akisimamia mtihani katika shule nyingine ya Mwangeza, aliandika baadhi ya maswali ya Kiswahili na Uraia kwenye simu yake ya mkononi na kumtumia Mkuu wa Shule yake ya Nkinto, Monica aliyekuwa shuleni kwake.
 
Baada ya Monica kupata maswali hayo, inadaiwa alitafuta majibu akiwa chooni huku wanafunzi wakimfuata huko huko na kupewa majibu.
 
Kamanda Kamwela alisema lengo lao lilikuwa kusaidia wanafunzi, wafanye vizuri katika mtihani wao wa kidato cha nne mwaka huu. Alisema wanafunzi waliishaambiwa wadanganye wanakwenda chooni, ili wakapewe majibu na Mkuu wa Shule.
 
"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa uvujishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya Monica na Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika shule tofauti.
 
“Baada ya Mkuu wa Shule kutumiwa maswali, alijificha chooni na watahiniwa kwa nyakati tofauti waliomba ruhusa kwa wasimamizi kwenda kujisaidia na hapo walimkuta Mkuu wa Shule na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali hayo," alisema Kamanda Kamwela.
 
Alisema baada ya Polisi kupata taarifa ya siri kutoka kwa wasamaria, iliweka mtego katika Sekondari ya Nkinto na kumkamata Mwalimu Monica huku simu yake ikiwa na baadhi ya maswali ya mtihani.

-Habari Leo

DARAJA LA SIFURI LIPO PALE PALE KATIKA SHULE ZA SEKONDARI YASEMA SERIKALI...NI BAADA YA WADAU KULALAMIKA KUWA KUFUTA SIFURI NI KAMA KUFUGA UJINGA...

SERIKALI imetangaza kurudisha daraja ziro katika elimu ya sekondari, huku zikiwa zimepita siku tatu, tangu uamuzi wa kufuta daraja hilo utangazwe.

Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kelele nyingi za wadau mbalimbali wa elimu, wakipinga hatua ya kufuta ziro na badala yake lisomeke kama daraja la tano.

Uamuzi wa kurudisha ziro ulitangazwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, huku mtihani wa kidato cha nne ukiwa umeanza jana.

Tamko la Mulugo limepingana wazi wazi na tamko jingine lililotolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifueni Mchome akitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro.

Kutokana na mkanganyiko huo, Bunge limeitaka Serikali kuwasilisha kauli moja kuhusu mabadiliko ya alama za ufaulu kwa shule za sekondari, ili kuondoa utata huo.

Mulugo alitoa tamko hilo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), ambaye alitaka kujua kama uamuzi huo wa Serikali ulilenga kuwasaidia wanafunzi wanaofeli.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema taarifa zilizoenea kuwa divisheni ziro imefutwa si za kweli.

“Serikali haijafuta divisheni ziro na wala hakuna divisheni V (daraja la tano), ipo divisheni I, II, III, IV na divisheni ziro kama kawaida,” alisema.

Alisema uamuzi wa kushusha madaraja uliofanywa haukuwa na lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofeli, bali ni kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.

Alisema Serikali imeweka madaraja mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi kutoka daraja moja kwenda jingine na kwamba hata hivyo alama za ufaulu bado ni 40 ambazo ni daraja la C.

Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia kati na kuitaka Serikali kuwasilisha bungeni kauli moja inayoeleweka, ili kuondoa utata unaowachanganya wananchi.

“Hii taarifa unayosema waziri ni tofauti kabisa na tamko la awali lililotolewa. Haiwezekani kuwe na taarifa mbili tofauti katika Serikali moja, nendeni mkakae mje na kauli moja inayoeleweka tusiwachanganye wananchi,” alisema Makinda.

Wakati Mulugo akitoa tamko hilo, zilikuwa zimepita saa tatu tangu kiongozi huyo anukuliwe katika vyombo vya habari akitetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kuanzisha daraja la tano.

Mulugo alifanya hivyo jana saa 1:40 asubuhi wakati akihojiwa katika kipindi cha kumepambazuka kinachorushwa na kituo cha Redio One, kinachoruka kila siku kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 4 asubuhi.

Katika kipindi hicho ambacho mada ilikuwa ni mfumo wa madaraja mapya, Mulugo aliutetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kudai kuwa hatua ya kupunguza viwango vya ufaulu imefanyika ili kupambanua madaraja hayo.

“Elimu zaidi inahitajika kwenye suala hili la mgawanyo wa madaraja, ukweli ni kwamba kilichofanyika katika kufuta alama ya ziro ni kupambanua madaraja ya ufaulu, ni suala ambalo litasaidia elimu yetu huko mbele ya safari,” alisema Mulugo.

Awali akijibu swali la msingi la Magige, Mulugo alisema Serikali haina mpango wa kuanzisha programu maalumu hasa za ufundi kwa wanafunzi waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.

“Kwa mwaka 2013, jumla ya wanafunzi 60,507 wa kujitegemea, wamejisajili kufanya mtihani huo, watahiniwa 3,578 wakiwemo wasichana 2,020 na wavulana 1,558 waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamejisajili kurudia mtihani huo,” alisema.

Mulugo alisema Serikali imekuwa ikiongeza na kuboresha vyuo vya ufundi na kuweka mazingira rahisi kwa wanafunzi ili waweze kupata stadi mbalimbali.

“Kati ya mwaka 2010 hadi 2012, Serikali kupitia VETA imesajili jumla ya Vyuo vya Ufundi Stadi 75 sawa na asilimia 75 na asilimia 10.8 ya vyuo 618 vilivyokuwepo.

“Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya vyuo 8 sawa na asilimia 3.2 ya vyuo 248 vilivyokuwepo vilisajiliwa na NACTE,” alisema Mulugo.

Mabadiliko hayo yameibua mjadala mkubwa, ambapo wasomi na wadau mbalimbali waliyaponda mabadiliko hayo na kudai kuwa yanaua elimu nchini.

Kwa mujibu wa wadau hao, uamuzi wa kufuta ziro sekondari ulikuwa umefanywa kisiasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kisiasa na si kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Walisema uamuzi wa awali ulilenga kutimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), ambao ni kuongeza ufaulu kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu kutoka asilimia 33 mwaka jana na kufikia asilimia 60
--Mtanzania

BAADA YA DR.MVUNGI KUVAMIWA NA KUKATWA MAPANGA...MAKAMU WA RAIS DR.BILAL AMJULIA HALI MUHIMBILI...

 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsikiliza Dkt. Mugisha Clement, aliyekuwa akimpa maelezo kuhusu alivyompokea Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, aliyelazwa  katika Kitengo cha Uangalizi Maalum (ICU) MOI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati alipokwenda kumjulia hali, kufuatia kujeruhiwa na majambazi usiku wa kuamkia jumapili huko nyumbani kwake maeneo ya Kibamba.

DK.SILAA AIBANA CCM...• Asema imeua elimu, ubunifu wa vijana...


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekuwa janga la Watanzania.
Amefafanua kuwa CCM inaua ubunifu wa vijana, kwamba asilimia 90 ya wanafunzi wanafeli shuleni huku viongozi wa chama hicho wakiwahadaa wananchi kwamba wanaleta maendeleo.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana alipozuru Shirika la Anga la Marekani (NASA) huko Huntsville nchini Marekani, ambako anaendelea na ziara yake ya kujifunza katika majimbo mbalimbali.
Akiongozana na mkewe, Josephine Mshumbusi, katibu mkuu huyo alilakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Charles Frank Bolden Jr. pamoja na watendaji wengine na kupata fursa ya kutembezwa sehemu kadhaa.
Dk. Slaa alifika hapo kujifunza mambo mbalimbali, ikiwamo namna ya kuwashirikisha na kuwapa vijana wa Kitanzania changamoto ili waweke jitihada zaidi kwenye masomo ya sayansi, waweze kuinyanyua Tanzania kutoka kwenye shimo la umaskini.
Taarifa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimnukuu Dk. Slaa akisema kuwa wanasayansi wa Kimarekani walifika mwezini baada ya kupata changamoto kutoka kwa aliyekuwa Rais wao, John F. Keneddy, aliyewaomba wanasayansi hao kufikisha mtu mwezini chini ya miaka 10.
Alisema kuwa wanasayansi hao walimjibu na kufika mwezini chini ya miaka minane. Hali aliyodai ilitokana na Serikali ya Marekani kuipa kipaumbele elimu.
Dk. Slaa alisema kuwa baada ya uhuru, hayati Mwalimu Nyerere aliipa kipaumbele elimu kwa ujumla. Akitolea mfano kwamba aliwachukua vijana watano wanajeshi na kuwapeleka nchini Ireland kusomea mambo ya uhandisi.
“Waliporudi walipelekwa Kibaha ambako walibuni na kutengeneza gari la kwanza lililoitwa Nyumbu, ambalo ni ubunifu wao.
“Baadaye Mwalimu Nyerere aliwabunia wanajeshi hao mradi wa dhahabu wa Buhemba, ambao ungewawezesha kulipia gharama za kutengeneza magari mengi,” alisema.
Katibu mkuu huyo aliongeza kuwa kwa bahati mbaya baada ya Mwalimu kustaafu, mafisadi walijipenyeza na kuuchukua mradi huo. Kwamba huo ndio ufisadi uliozaa Meremeta.
“Mradi wa Nyumbu ukafa na kilichotokea ni ufisadi wa sh bilioni 155 uliohusisha Benki ya Netherlands ya Afrika Kusini. Hadi leo hakuna maelezo licha ya fedha hizo kutumika kwenye kampeni za CCM za mwaka 1995,” alisema.
Dk. Slaa alihoji ni maendeleo gani wanazungumzia CCM wakati watoto hawajui kusoma wala kuandika, huku wanajeshi waadilifu, wabunifu, wazalendo na wanaojituma wamefikia kuishi maisha ya ajabu.
“Ubunifu wao kama mradi wa Nyumbu umeuawa na CCM, imefanya maisha yao kuwa magumu na ya kusikitisha. Wanajeshi waliostaafu wamebaki kama ombaomba.
“Wale wanaoshiriki kulinda amani nje ya nchi wanadhulumiwa hela zao pale wanaporudi Tanzania. Nchi ambayo haiwezi kuwahudumia wanajeshi wake ni nchi isiyofaa kuwa katika ramani ya dunia,” alisema.
Dk. Slaa aliwaomba wanajeshi na vijana kutokata tamaa wala kusikitika kwani CHADEMA inasikia vilio vyao, na kwamba wanatambua kuwa ugumu wao wa maisha umesababishwa na CCM.
“Wakati hao CCM wanajineemesha na hela zetu za kodi, wanajeshi na wananchi kwa ujumla wanashindwa hata kujenga nyumba ya kujisitiri punde wanapostaafu,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM imeua ubunifu ndani ya Tanzania na kuamua kuwaweka vijana kuwa mazezeta ili waendelee kuwatawala.
“Wenzetu wanapeleka watu mwezini, lakini Watanzania hata wembe tunanunua kutoka nje kwa sababu ya CCM. Wakiendelea kuwanyima wananchi haki zao za msingi muda utafika watachoka,” alisema.ima
-tanzania daima

MAKUBWA: WANAFUNZI WA NGUVUMALI JIJINI TANGA WAFANYA MAPENZI CHOONI NA MADARASANI...




 
SHULE ya Sekondari Nguvumali wilayani Tanga, inadaiwa kukumbwa na pepo la ngono baada ya wanafunzi wake kubainika wakifanya ngono hovyo chooni, madarasani na njiani  wakati wa kwenda na kurudi kwenye makazi yao.
Hali hiyo inadaiwa kusababishwa na kushuka kwa kiwango cha elimu shuleni hapo.
 
Tatizo hilo liliwekwa hadharani jana na Diwani wa Kata ya Nguvumali, Mustafa Seleboss   na Mwenyekiti wa Nguvumali Agness Milambo, kwenye bonanza la kampeni za uzinduzi wa kupinga ukatili mashuleni lililoandaliwa na asasi ya kiraia ya Tree of Hope ya jijini Tanga.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa Kata ya Nguvumali, walisema asilimia 80 ya wanafunzi wa Sekondari ya Nguvumali wanafanya mapenzi hovyo hata darasani, vyooni na vichakani wakati wakienda au kurudi nyumbani.

Baadhi ya wanafunzi  shuleni hapo, Peter Chambai, Hassan Saidy na Teresia John, wamekiri kufanyika kwa vitendo hivyo viovu, ambavyo wameviita ni ukatili na unyanyasaji  wa kisaikolojia dhidi ya wanafunzi wasiopenda mchezo huo mchafu.
 
Wanafunzi hao walisema washiriki wa vitendo hivyo ni wanafunzi kwa wanafunzi  au walimu kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tree of Hope, Fortunata Manyeresa, ameahidi kuingia mtaa kwa mtaa kuwasaka  wanafunzi wanaojihusisha na  vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo ili wanaowarubuni wachukuliwe hatua.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger