Mvomero.Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala juzi aliwekwa kitimoto na baadhi ya wakulima wilayani Mvomero mbele ya mawaziri wengine wanne katika mkutano ulioitishwa kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mkindo.
Makala ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero ulipo
mgogoro huo, alilalamikiwa na wakulima hao wakidai kwamba amekuwa
akiwasikiliza zaidi wafugaji na kutoonyesha
jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo kwa
agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chizza, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck
Ole-Medeye.
Akijibu shutuma zilizoelekezwa kwake, Makala
alisema: “Msiseme tu mwangalie na juhudi zangu. Namshukuru Dk Nchimbi
kwa kusoma barua ya Waziri Mkuu, uongo umejitenga na ukweli
umedhihirika. Mimi nikiwa mbunge ni mwakilishi wa wananchi, nimewaita
mawaziri hapa, nimekuwa kama mshenga ili wasikie malalamiko yenu,”
alisema Makala.
Malalamiko ya wananchi
Katika malalamiko yao, wakulima hao walisema licha
ya uonevu wanaoupata kutoka kwa wafugaji na Jeshi la Polisi, mbunge wao
amekuwa kimya.
“Mbunge wetu hatusaidii kitu kila tunapopata
matatizo. Yalipotokea machafuko Kijiji cha Hembeti hakuonekana. Kuna
taarifa zisizo rasmi kuwa amekuwa akifanya mapatano na wafugaji kwa
siri,” alisema mmoja wa wanakijiji wa Mkindo, Shomari Msumi na kuongeza:
“Watoto wetu wamelazwa Hospitali ya Bwagala,
Polisi wamekuja kuwafunga pingu na kuondoka nao, wafugaji hawaguswi kwa
sababu ya nguvu ya fedha. Vyombo vya Dola hasa Mahakama nayo
inatukwamisha. Mazao yameliwa lakini kesi haziamuliwi, hadi leo kesi iko
wilayani.”
Mkulima mwingine, Aziz Dendego alisema:
“Tunaumizwa mno na viongozi wa wilaya. Mimi nimefika hapa mwaka 1975.
Kero zimeanza miaka 20 iliyopita na Serikali ndiyo inayosababisha. Mkuu
wa Mkoa anaagiza tu lakini hatuoni vitendo. Mkuu wa wilaya alikuwa mzuri
lakini sasa amebadilika kabisa. Bunduki za kijeshi zimetumika kwenye
mapigano, wakulima wamezipataje?”
Mmoja wa wakulima hao, Shaaban Khamis alisema
wameamua kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi baada ya kulalamika kwa
muda mrefu bila kusikilizwa.
Wakulima hao pia wamemlalamikia Mwenyekiti wa
Kijiji cha Wafugaji cha Kambala waliyemtaja kwa jina moja la Kashu
wakidai kuwa amekuwa akiongoza mapigano dhidi ya wakulima.
--Mwananchi
--Mwananchi