
Tindikali ikiwa katika ndoo tayari kwa kuuzwa, uchunguzi umebaini kuwa bidhaa hii hatari huuzwa kiholela jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Siku chache baada ya wasichana
wawili raia wa Uingereza kumwagiwa tindikali mjini Zanzibar, imebainika
kuwa, tindikali za aina mbalimbali zinauzwa kiholela kama njugu jijini
Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha
kuwa jijini Dar es Salaam yapo maduka mengi yanayouza tindikali ya kila
aina na bidhaa hiyo inauzwa bila ya udhibiti wowote kuanzia Kariakoo
hadi Vingunguti.
Wiki iliyopita, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Samwel Manyele alitoa miezi mitatu kwa wafanyabiashara wa tindikali
kujisajili ili kuzuia kuongezeka kwa matukio ya uhalifu kwa kemikali
hiyo nchini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mitaa
ya Dar es Salaam, umebaini kuwa tindikali za aina mbalimbali
zinapatikana kwa wingi katika maduka ya rejareja na jumla, huku wauzaji
wa bidhaa hizo wakishindwa kutoa tahadhari yoyote kwa wateja wao.
Imebainika kuwa tindikali zinazopatikana kwa
urahisi zaidi ni Sulphonic Acid ambayo imetajwa kutumika kutengeneza
sabuni za maji (multipurpose detergents), Sulfuric acid inayotumika
kutengeneza maji ya betri na Hydrochroric acid inatumiwa na
wajasiriamali kutengeneza dawa za usafi.
Kemikali nyingine ambayo imeelezwa na watumiaji
wake kuwa ni hatari ni Hydrogen Peroxide ambayo hutumika kusafisha
mafuta ya mawese yanayotumika kutengenezea sabuni za kipande.
Katika Mtaa wa Gerezani Kariakoo, kuna duka
maalumu la kuuza kemikali mbalimbali kwa bei ya rejareja na jumla,
kemikali hizo zinauzwa kati ya Sh4,000 hadi Sh6,000 kwa kilo moja
kutokana na aina yake.
Muuza kemikali mmoja katika mitaa ya Sinza
wilayani Kinondoni, ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini kuhofia
usalama wake, alisema biashara hiyo ilianza kushamili miaka mitatu
iliyopita baada ya kuanzishwa kwa mafunzo ya kutengeneza bidhaa
mbalimbali zinazotumia kemikali.
“Matangazo yanayotolewa katika vyombo vya habari
kuhusu ujasiriamali wa kutengeneza sabuni aina mbalimbali, ndiyo
yaliyochochea kuongezeka kwa mahitaji ya tindikali hapa nchini. Kwa
mfano, (anamtaja mhusika) anafundisha namna ya kutengeneza maji ya betri
za magari kwa kutumia Sulphuric acid, unategemea wajasiriamali
wakanunue wapi hiyo tindikali?” anahoji.
Matukio ya kujeruhiwa na tindikali
Agosti 7 mwaka huu raia wawili wa Uingereza, Kate
Gee na Kirstie Trup wote miaka 18 walishambuliwa kwa tindikali na watu
wasiojulikana wakati wakitembea kwenye mitaa ya Stone Town mjini
Zanzibar. Raia hao walisafirishwa na kurudishwa Uingereza ambako
wanaendelea na matibabu.
Kabla ya kuondoka nchini, Rais Jakaya Kikwete
aliwatembelea raia hao hospitali na kusema kuwa tukio hilo limeitia aibu
nchi kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha
linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
-mwananchi
-mwananchi