ONGEZEKO kubwa la wahamiaji haramu wilayani Ngara mkoani Kagera
linatokana na Watanzania kuamua kuoa wanawake wa Rwanda kuliko Watanzania kutokana
na kutozwa mahari kidogo na kuvutiwa na uzuri wa wanawake wa Kinyarwanda,
Imeelezwa.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta ameahidi kuwasilisha ombi maalumu kwa Rais Jakaya Kikwete ili wanawake wa
Rwanda waliokuwa wameolewa nchini na kukumbwa na Operesheni Kimbunga, warejee
nchini kuungana na familia zao lakini kwa kuhalalisha ukaazi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constatine Kanyasu aliyekuwa akisoma taarifa ya
utekelezaji wa Operesheni Kimbunga awamu ya kwanza iliyohusisha mpaka wa Rusumo
unaozitenganisha Rwanda na Tanzania, alisema kumekuwepo na ongezeko kubwa la
wanaume wa Tanzania kuoa wanawake wa Rwanda kutokana na udogo wa mahari na
uzuri wa Wanyarwanda.
Alisema hata hivyo pamoja na kupendezewa na vitu hivyo kwa wanawake wa
Kinyarwanda lakini wanaume hao wa Tanzania wanashindwa kuwalipia wake zao hao
ada ya Dola za Marekani 550 ( Sh 880,000) zinazotozwa kila baada ya miaka
miwili ili kuhalalisha ukazi wao nchini kutokana na kutobadili uraia kuwa
Watanzania.
“Waziri (Sitta) sababu kubwa wanayoitoa wanaume wengi wilayani hapa
(Ngara) kama sababu ya Watanzania wengi kuamua kuwaoa Wanyarwanda ni kutozwa
mahari kidogo sana kuliko ile inayotozwa ili kumuoa mwanamke wa Tanzania.
Inasemekana kuna familia wanapokea hadi kuku, mbuzi au fedha kidogo ili
kuruhusu mtoto wao kuolewa.
“Kwa vile wanapenda kuwa na wake na kwa vile hawana uwezo wa kifedha wa
kutoa mahari kubwa uamuzi wanaofikia ni kuoa wanawake wa Kinyarwanda, lakini
kwa kufanya hivyo wanajikuta pia wanashindwa kuwalipia wake zao ada hiyo ya
ukazi na kuwafanya kuishi nchini kinyume cha utaratibu,” alisema Mkuu huyo wa
Wilaya.
Alisema kutokana na hatua hiyo Operesheni Kimbunga imewakumba wanawake
wengi waliokuwa wameolewa nchini hatua iliyosababisha kubakia kwa watoto
wasiokuwa na mama wa kuwalea na inayozorotesha uhusiano wa kifamilia na mataifa
ya Rwanda na Tanzania.
Alisema wakati maofisa wa Serikali wa pande hizo mbili walikuwa na
kawaida ya kukutana kila baada ya miezi mitatu kuzungumzia masuala mbalimbali
ya ushirikiano na usalama, tangu kuanza kwa Operesheni Kimbunga vikao hivyo
havifanyiki.
Akizungumzia kuondoka kwa wanawake walioacha familia zao, Waziri Sitta
ambaye pia alikiri uzuri wa wanawake Wanyarwanda alisema atawasilisha pendekezo
kwa Rais Kikwete ili waweze kuruhusiwa kurejea nchini na kufuata taratibu za
ukazi halali ili kuweza kulea familia zao.
“Hatuna ubaya na watu wa Rwanda hata chembe na tunaomba walielewe
hilo.Operesheni Kimbunga imewakamata pia Wahindi, Wamalawi, Wachina na hawa
Wamakonde maana wapo Wamakonde wa Kusini mwa Tanzania lakini wapo Wamakonde wa
Kaskazini mwa Msumbiji hawa pia wamekumbwa na operesheni hii.
“Ikumbukwe kwamba ni haki ya kila nchi kuendesha operesheni ya kuhakiki
ukazi wa wahamiaji. Ila kwa sababu ya ujirani mwema na hasa kwa kuzingatia hili
la wanawake kuacha familia zao nitapeleka mapendekezo kwa Rais tuweze
kurekebisha maana tunabanwa pia na mikataba ya kimataifa inayohusu haki za
binadamu na watoto,” alisema Sitta.
Akizungumzia malipo ya Dola 550 kila baada ya miaka miwili zinazopaswa
kulipwa ili kuwezesha mke asiye raia kuishi nchini, Waziri Sitta alisema ni
vizuri kiwango hicho kikaangaliwa upya kutokana na ukweli kwamba wanaume wengi
wanaokimbilia Rwanda kuoa wanakwepa ukubwa wa mahari nchini Tanzania kwa kutokuwa
na uwezo.
“Nadhani kuna umuhimu wa kuangalia upya kiwango hiki, maana kwa mtu
asiye na uwezo kulipa ada hiyo tena kwa Dola ya Kimarekani kunaweza kuwa ni
chanzo cha kukwepa sheria na taratibu za nchi yetu. Lengo si kuwafukuza wenzetu
bali kuwataka wafuate sheria,” alisema.
Akizungumzia wahamiaji haramu waliorejeshwa makwao, Kamanda wa Uhamiaji
Rusumo, Samwel Mahilane alisema hadi kufikia Oktoba mosi mwaka huu, wahamiaji
haramu 7, 858 walirejea makwao kwa hiari kupitia mpaka wa Rusumo, huku
wahamiaji 2,890 wakirejeshwa kwa nguvu na kufanya jumla ya wahamiaji waliorejea
nchini Rwanda kufikia 10,348-habarile