WAKATI mchakato wa Katiba Mpya ukitajwa kutaka kuhujumiwa na
moja ya mitandao ya urais katika Chama cha Mapinduzi (CCM) ili pamoja na mambo
mengine kumkomoa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
amegeukwa huku watu wanaodhaniwa kumuunga mkono kisiasa wakiumbuliwa na wenzao.
Lowassa amegeukwa baada ya kutolewa kwa tamko kupinga kitendo
chake cha kufanyiwa mila za kijadi (tambiko) na wana-ukoo wa Mtemi wa
Unyanyembe, ukoo unaohusishwa na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Kwa mujibu wa tangazo rasmi lililochapishwa katika gazeti hili,
Septemba 14, mwaka huu, Lowassa ambaye anatajwa kuweza kuwania urais katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alifanyiwa mila za kijadi (tambiko) akipewa
heshima ya kuwa chifu wa Wanyanyembe, jambo ambalo sasa linadaiwa kufanyika
bila ridhaa ya wanaukoo husika.
Kutokana na hali hiyo, tamko rasmi la Wanyanyembe la kupinga na
kulaani tukio hilo limetangazwa huku sehemu yake kubwa likimpigia chapuo Waziri
wa Afrika Mashariki, Sitta, ambaye awali, baada ya Lowassa kupewa hadhi ya
chifu wa Wanyanyembe, taarifa zilisambazwa kwamba ameisambarartisha moja ya
ngome za Waziri Sitta.
Hali hiyo ya siasa za ndani ya CCM kupenyezwa katika koo za
kichifu inaandika historia mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,
ikitabiriwa ya kwamba vituko zaidi vinaweza kuibuka na hasa ndani ya CCM,
chenye jukumu la kuteua mgombea wake wa urais katika mazingira ya siasa za
ushindani ambazo mara kwa mara, zimekuwa zikitawaliwa kwa mizengwe na hila.
Ili kuthibitisha msuguano wa kisiasa unaovuka mipaka ya vyama
ambao sasa unazama katika koo za kichifu, tamko hilo la Wanyanyembe linaeleza:
“Kusema Mhe. Lowassa Mbunge wa Monduli kavunja ngome ya Mhe. Samuel Sitta ni
utashi wa kijinga. Mhe. Samuel Sitta ni Mnyanyembe na jina lake kwa upande wa
Utemi anaitwa Ifuma, Itetema ni kwake. Babu yake wa kumzaa mama yake Hatat
Kagoli Said Fundikira, wajomba zake Mtemi Nassoro S. Fundikira, Mtemi Abdallah
S. Fundikira, mama, wajomba zake wamezikwa Itetema.”
Lowassa ambaye alijiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008, kwa
kuhusishwa na kashfa ya mradi wa umeme uliokabidhiwa kampuni ya Richmond
Development LLC, hakuwa tayari kuzungumzia hatua hiyo ya kugeukwa.
Raia Mwema
ilimtafuta Lowassa kutaka kujua ni namna gani aliweza kupewa hadhi ya uchifu wa
Unyanyembe katika mazingira hayo tata na kama kweli kuna nguvu ya fedha
ilitumika ili kufanikisha tukio hilo lakini Lowassa alipopatikana kwa simu
alijibu; “Nipo nje ya nchi,” Na kukata simu.
Hujuma ya Katiba Mpya CCM
Katika hatua nyingine, zimekuwapo habari kwamba ndani ya CCM
kumekuwapo na kundi maalumu lenye malengo ya kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya
ili hatimaye Katiba ya sasa iendelee kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015
kutokana na maandalizi yao kuingiliwa ikiwa kutakuwapo na serikali tatu.
Inaelezwa kwamba kundi hilo ambalo tayari lina mgombea wake wa
urais ambaye amefanikiwa kujenga mtandao ndani ya CCM, serikalini na kwa baadhi
ya wadau wakuu wa sekta binafsi, linapigania kuendelea kutumika kwa Katiba ya
sasa katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015 kwa sababu kukubali Katiba Mpya maana
yake ni kuvuruga mtandao wao wa urais, ili hali muda waliotumia kujenga mtandao
huo ni mrefu na uliogharimu fedha nyingi.
Chanzo chetu cha habari kutoka CCM kinaeleza kwamba mtego mkubwa
wa kundi hilo umewekwa katika Bunge la Katiba ambamo kati ya wajumbe wanaounda
Bunge hilo ni wabunge wa CCM ambao wengi wamo katika kundi hilo na wanamuunga
mkono mgombea huyo anayetajwa kutokea mikoa ya Kanda ya Kaskazini mwa nchi.
“Bado kuna kilio kwamba mchakato huu wa Katiba Mpya si wazo la
Chama cha Mapinduzi bali ni mchakato binafsi wa Rais Kikwete, na utaona
alitangaza kuanza kwa mchakato huu kabla ya kukishirikisha chama chake. Na hili
lilijitokeza katika kikao cha wabunge wa CCM hivi karibuni mjini Dodoma, wapo
waliodiriki kusema Katiba Mpya haimo katika Ilani ya CCM na kwa hiyo jambo la
muhimu kwao ni kutekelezwa kwa Ilani ya Uchaguzi,” kinaeleza chanzo chetu cha
habari ndani ya CCM.
Kundi hilo linaanza kubainika katika wakati ambao tayari Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe akishinikiza mchakato huo wa Katiba usonge
mbele na kama Rais Kikwete asiposaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, atamshangaa na kimsingi, Rais anaweza kuingia
katika mgogoro na Bunge.
Lakini wakati Waziri Chikawe akisema hayo, chanzo chetu kingine
cha uhakika cha habari kinaeleza kwamba uongozi wa CCM kwa sasa, chini ya
Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana, hautaweza kumudu kuwatuliza wabunge wa chama
hicho kama ikitokea Rais Kikwete hatosaini muswada huo.
Kutokana na hali, taarifa za uhakika zinaeleza kwamba Rais
Kikwete ambaye amerejea nchini Jumatatu wiki hii, atasaini muswada huo lakini
pia ili kutuliza msuguamo kuhusu Katiba Mpya na hasa wakati huu wa kuelekea
katika Bunge la Katiba, muswada huo baada ya kusainiwa na Rais na kuwa sheria,
sheria hiyo itarudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho madogo.
Kati ya marekebisho madogo yanayoweza kupendekezwa kufanyika
katika mkutano ujao wa Bunge unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15, mwaka huu kabla
ya kuitishwa kwa Bunge la Katiba Novemba, mwaka huu, ni pamoja na kuiongezea
uhai Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ili
iwepo hadi wakati wa mchakato wa kura za maoni kuhusu Katiba Mpya.
Hata hivyo, wakosoaji wa kuendelea kuwapo kwa Tume hiyo wamekuwa
wakieleza kwamba hawaoni mantiki ya Tume hiyo kuendelea kuwapo kwa sababu
wakati wa kura ya maoni, wananchi wataulizwa swali na kujibu Ndiyo au Hapana,
na jibu lolote kati ya hayo ni jibu sahihi, na wanahoji Tume iwepo ili kufanya
nini?
Pia wakosoaji hao wanasema kiutaratibu Tume za Rais humaliza
muda wake baada ya kukabidhi ripoti kuhusu kazi waliyopaswa kuifanya, wakirejea
Tume mbalimbali za Rais, kuanzia ile ya Jaji Francis Nyalali na nyinginezo.
Mawaziri wajibu mapigo ya wapinzani
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Mary Victor, anaripoti
kwamba, mawaziri watatu wa serikali ya Rais Kikwete wamejibu makombora
waliyotupiwa na vyama vya upinzani – wakisema hawana mpango wowote wa kujiuzulu
kama wanavyoshinikizwa.
Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano
na Uratibu) , Stephen Wassira , Waziri wa Katiba na Sheria , Mathias Chikawe na
Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Vyama vya upinzani vilidai kwamba mawaziri hao wanapaswa
kujiuzulu kutokana na msimamo wao wa kumtaka Kikwete asaini Muswada wa
Marekebisho ya Katiba unaopingwa na vyama hivyo kwa ajili ya kuepusha kuvunjika
kwa Bunge.
Katika mazungumzo waliyofanya na gazeti hili kwa nyakati tofauti
wiki hii, mawaziri hao walisema hawajafanya jambo lolote kinyume cha utaratibu
na madai ya kuwataka wajiuzulu hayana maana yoyote.
Kwa upade wake, Wassira alisema; “Nijiuzulu kwa lipi haswa? Kwa
sababu nina mawazo tofauti na wapinzani? Yaani nchi hii siku hizi ukiwa na
mawazo tofauti na wapinzani basi ujiuzulu. Mimi nasema, basi na wao wajiuzulu
kwa sababu wametofautiana na mimi.
“Jambo la msingi ambalo nataka kuliweka wazi hapa ni kwamba
wapinzani walipoteza haki ya kuupinga huu muswada mara baada ya kuamua kukimbia
bungeni. Pale ndipo mahala pekee ambako sheria zinatungwa.
“Sheria hazitungwi Ikulu wala kwenye viwanja vya Jangwani. Sasa
wao sehemu halali ya kutunga sheria wanazira halafu wanataka sheria zikatungwe
na Rais Ikulu au na wananchi pale Jangwani. Haiwezekani, alisema mwanasiasa
huyo mkongwe.
Kwa upande wake, Chikawe alisema kwa ufupi, “Siwezi kujiuzulu
kwa sababu ya kusema ukweli. Hivi Rais akiusaini muswada huo watamtaka
ajiuzulu pia? Siwezi kujiuzulu kwa sababu ya kusema ukweli. Naijua katiba
na nakijua kifungu hicho, wakiseme chote vizuri wasiwapotoshe ninyi na
wananchi.”
Kifungu anachokizungumzia Waziri ni kile kilichozungumzwa na
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho,
John Mnyika aliyesema ““Wassira, Chikawe na Simba kama wana hofu kwamba Bunge
litavunjwa iwapo muswada utarejeshwa mara ya tatu na wao watapoteza nafasi zao
za uwaziri.”
Naye Sophia Simba alipoulizwa na Raia Mwema ikiwa yupo tayari
kujiuzulu, alisema “Hao wapinzani wanachanganyikiwa . Mimi sijazungumzia hayo .
Mimi nilizungumza kuhusu kauli ya Mbowe ya kuitaka jamii kutotii sheria. Hao
hawastahili kuitwa viongozi kwani wanachochea fujo ndani ya jamii”
Msimamo wa vyama hivyo kumtaka Rais asiusaini muswada, umetokana
na baadhi ya vifungu kuingizwa kinyemela kwenye muswada uliowasilishwa bungeni
na pia madai kwamba mchakato mzima umehodhiwa na CCM.
-RAIA MWEMA