·
Msemaji akanusha na
kuahidi mafanikio zaidi
ZIKIWA zimebakia wiki tatu kukamilika kwa awamu ya pili ya
operesheni Kimbunga dhidi ya wahamiaji haramu, ziko dalili za kushindwa
kuwakamata wahamiaji haramu wafugaji wanaotuhumiwa kuharibu mazingira kutokana
na wingi wa mifugo yao.
Taarifa kutoka ndani ya wana-operesheni hiyo na Serikali ya Mkoa
wa Kagera zinaeleza kuwa operesheni hiyo inapambana na ugumu katika kuwakamata
wafugaji hao matajiri kwa sababu imedhihirika kuwa wana vibali vya uraia.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa anayeshiriki katika operesheni
hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, imedhihirika kwamba watu hao
walipewa uraia bila kwanza kuukana uraia wa nchi zao kama sheria
inavyotaka, hali inayowafanya kuwa raia wa nchi mbili, wakiwa Tanzania wanakuwa
raia na wakiwa kwao ni raia, na wakati huu wa operesheni wote
wamekimbilia nchini Rwanda.
"Ili tufanikiwe kukomesha hali hii ninachoweza kushauri ni
kumuomba Rais au baada ya operesheni hii ashauriwe kubatilisha hati za uraia
wao, ili tuwafanyie uchunguzi makini kulingana na mienendo yao kabla ya kuwapa
uraia tena na wakubali kuukana uraia wa nchi zao," anasema ofisa huyo.
Anasema operesheni hiyo imefanikiwa kuwaondoa baadhi ya
wahamiaji haramu, lakini ukiipima kwa mantiki ya kuondoa wahamiaji
wanaosababisha athari kwa mazingira na usalama wa wananchi ni vigumu kusema
operesheni imefanikiwa.
"Bila kuwachambua akina nani walipewa uraia kwa kufuata
taratibu na kuwachambua upya, hali inavyoonyesha itakuwa vigumu sana mikoa hii
ya Kagera, Kigoma na Geita kutulia, tutakuwa tunafanya operesheni kwa gharama
kubwa lakini baada ya muda hali inajirudia, tunahitaji kuwachambua hawa watu
upya," anafafanua ofisa huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasulo mkoani Kagera,
Yusufu Katula, kijiji kilichoathirika kwa kukaliwa na wahamiaji haramu, anasema
baadhi ya wahamiaji haramu wanapitiwa vibali vya uraia bila serikali ya kijiji
kushirikishwa.
"Kwa watu ambao tunawajua kabisa kuwa ni wahamiaji haramu
na ambao tumewaripoti kwa serikali ni wawili tu ninaweza kusema kwa uhakika
wamerejeshwa Rwanda, wengine nasikia wamepewa uraia, sijui kilitokea
nini," anasema Katula.
Chanzo chetu kingine kutoka ndani ya Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa
Kagera kilieleza kuwa wapo baadhi ya wafugaji hao matajiri waliokamatwa lakini
ilibidi waachiwe kwa sababu walikuwa na vibali vinavyoonyesha ama ni raia au
wanaishi nchini kihalali.
Raia Mwema
lilipomtafuta Kiongozi wa Operesheni hiyo, Kamanda Simon Siro, Jumatatu wiki
iliyopita, alisema hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo hadi Jumatano wiki hii,
siku ambayo gazeti hili tayari linakuwa limekwishachapishwa na kusambazwa.
Kwa upande wake kiongozi wa Timu ya Habari na Mawasiliano ya
Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa, amesema operesheni hiyo ni endelevu na
hakuna mtuhumiwa atakayeachwa.
"Napenda kukuhakikishia kuwa operesheni ya kuondoa
watu wanaoishi nchini isivyo halali sambamba na majambazi, majangili,
silaha zinazomilikiwa isivyo halali, wafugaji haramu ni endelevu. Tuko katika
awamu ya pili ambayo inakwenda hadi Oktoba 20, mwaka huu. Hakuna
mtuhumiwa atakayeachwa bila kuchukuliwa hatua ili kuthibitisha uraia wake na
serikali kuridhika na uthibitisho huo," alisema Zamaradi Kawawa.
Wakati operesheni Kimbunga inaanza gazeti hili liliandika habari
ya wananchi wa Mkoa wa Kagera kutokuwa na imani juu ya operesheni hiyo na
kueleza kuwa kipimo cha mafanikio ya operesheni hiyo itakuwa ni kuona kama
wahamiaji haramu ambao pia ni wafugaji matajiri wataondolewa, huku
wakimtaja kigogo mmoja ambaye walisema bayana kuwa kama haitamgusa kigogo huyo,
basi haitakuwa na maana.
-raia mwema