Rais
wa Uganda, Yoweri Museveni amesema hana mpango wa kumuandaa mwanawe
kuwa rais wa nchi hiyo kwa kuwa Uganda si nchi iliyo chini ya utawala wa
kifalme.
Kauli
hiyo ya Rais Museveni imehitimisha msimamo wake kuhusu taarifa
zilizokuwa zikieleza kwamba ana mpango wa kumrithisha kiti hicho
mwanawe, Brigedia Muhoozi Kainerugaba mara atakapoadchia madaraka.
Akizungumza
na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, Museveni alisema “Kijana huyu
ni ofisa wa jeshi ambaye wala hana mpango na siasa.” Na hata hajawahi
kuonyesha kufikiria kuingia kwenye siasa kwa siku za hivi karibuni.
Katika
mahojiano hayo yaliyorushwa usiku wa kuamkia juzi wakati akiwa kwenye
mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Museveni
alisema kwamba Brigedia kainerugaba hataweza kuingia kwenye siasa “kwa
kipindi kifupi kijacho.”
Kwa
sasa, Brigedia Kainerugaba ni mkuu wa kikosi maalumu cha wataalamu wa
jeshi wanaoilinda familia ya Rais na kuweka mifumo ya kisasa ya ulinzi
nchini humo.Kusoma zaidi bofya
Alipoulizwa
iwapo mwanaye huyo wa kwanza anastahili kuwa rais ajaye baada yake,
alisema: “Hiwezekani kwa kuwa hana mapenzi na siasa. Pia Uganda si nchi
ya kifalme hivyo hawezi kurithishwa, tunategemea uchaguzi. Haiwezekani
kuhamishia urais kwake. Kiongozi yeyote wa kisasa analazimika
kuchaguliwa kupitia uchaguzi unaokubalika.”
Museveni
ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 27 alisisitiza kwamba hata iwapo
mwanaye huyo ataonekana kuvutiwa na kuingia kwenye siasa katika kipindi
kirefu kijacho, itakuwa ni juu yake na watu wa Uganda kuhusu kuingia
katika wadhifa wa urais.
Mahojiano
hayo yalilenga kupata kauli ya Museveni kuhusu taarifa zilizotolewa Mei
mwaka huu kwamba Breigedia Kainerugaba anaandaliwa kwa ajili ya
kurithishwa nafasi ya baba yake, hivyo amekuwa akipandishwa vyeo kwa
kasi jeshini ‘kwa sababu maalumu’.
Taarifa
hizi zilitolewa kwa umma baada ya kunaswa kwa waraka wa aliyekuwa mkuu
wa Usalama wa Taifa, Jenerali David Sejusa kwenda kwa wakuu wengine wa
usalama kutoa maelekezo juu ya hatua hiyo.
Jenerali Sejusa aliandika barua kwenda kwa mkuu wa vyombo
vya usalama vya serikali akitaka kujua kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya
maofisa wa serikali akiwemo yeye wamekuwa wakipinga mkakati wa kumuandaa
Muhoozi hivyo kuundiwa mkakati wa kuwekwa kando.