Hotuba kamili ni hii:
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA,
2013
Ndugu
Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha
kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu
mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa
safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali
nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada
ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee
baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya
mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno.
Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu
Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano
wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika
Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili
kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul
Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika
Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi
zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si
ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze
mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano
mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa,
watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi
kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na
watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu
Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa
tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya
kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao
na silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali
halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku
14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya
hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu
Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi
nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari.
Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102
zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013
na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828
walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa kutumia
silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive
hand grenades), silaha 80, risasi 780
na mitambo 2 ya kutengeneza magobole
vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa
katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105
zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu
Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au
waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya
nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza
wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia
tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya
Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa
kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka
kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi.
Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la
Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.
Ndugu
Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka
mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku zote
Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka
mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia.
Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka
wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia
nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa,
ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu
Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa
nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au
kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao.
Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza
watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika
kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti,
taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua
zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa
Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi
kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza Makamanda na
askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, Idara ya
Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali
kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe
20 Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa
endelevu, muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee
kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu
Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba,
2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada na Marekani. Nchini
Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya
Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo
na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto
zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo hicho
wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na Elimu,
Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro na
Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na viongozi wa
vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu
Wananchi;
Nchini Marekani nilikutana na
kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo
Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Mazungumzo
yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda
vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana
na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa
kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni
2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji
umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa
sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu
Wananchi;
Jambo lingine kubwa na la faraja
kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini za
kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za
Milenia yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na
Bodi ya MCC na kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili
hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo lingine muhimu katika safari
yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na “International Congressional
Conservation Foundation” kwa kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori
na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana
nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada tunazozifanya
sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama na
misitu.
Ndugu
Wananchi;
Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za
utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo
na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa
kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu
Wananchi;
Shabaha kuu ya safari yangu ya
Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea
jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni
kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani: Post
2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama
mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo,
mjadala huo unaanza kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane
ya Milenia ya mwaka 2000 umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015
kwa kila nchi na kwa dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa
kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika kila nchi.
Yapo malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo
upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo
ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia
shabaha katika mambo yafuatayo:
- Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
- Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
- Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
- Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
- Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu
Wananchi;
Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5
ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015.
Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini
na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua
tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa
chakula na kuongeza mapato ya wakulima. Mafanikio yanaanza kuonekana
lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015.
Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash
Transfer ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama
tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado
tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia
namba 5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza
vifo vya kina mama wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua
chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha
ifikapo mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017)
una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati,
vituo vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana
mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha
hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza
mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya lengo. Miaka michache ijayo,
tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu
Wananchi;
Lengo la Milenia namba 8 linazihusu
nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza
Malengo ya Milenia. Bahati mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango
wanavyotarajiwa kutoa na hata vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa
mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya
Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu
Wananchi;
Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa
Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani iliyofanikiwa
kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi
wote waliozungumza ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za
kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la
upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka
2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya
utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya
baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu
Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21
Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara
la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza
maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma
salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa
Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo
watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya
msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini
ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza
maisha.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu
shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali.
Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na
Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili
hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na
kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea
nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote
wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli,
migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia
waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and
x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini
gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu
Wananchi;
Nawaomba muendelee kufanya shughuli
zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari.
Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha
kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na
taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea
kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi
Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa
nchi yetu na watu wake.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu
Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba,
2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda
taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na
imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea
maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni
ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa
mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge
Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya
Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia
kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba
Mpya.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011
kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria
hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na
Chama tawala. Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo
pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa
marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum
na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko
yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa
vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na
maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali
ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu
Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi
wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba
kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70
zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90.
Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu
Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa
Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba,
Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau
na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa
kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe wa
Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe
wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba
mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na
Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu
Wananchi;
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama
vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo
mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi.
Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa
maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke
Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa
Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa
Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani,
Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu
Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni
yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo
hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi
ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja
hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali
isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa
wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya
kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya
Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa
mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea
kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya
hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi
ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa
yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Ndugu
Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya
Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake
wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada
Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema
mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi
nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge
ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi
nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa
Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii.
Naamini na wao wanautambua ukweli huo.
Ndugu
Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia
hujirudia”. Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012.
Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja
moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi.
Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na
kumaliza mzozo.
Ndugu
Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta
ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya
lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji
dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia
ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria
au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata
Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu
wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na
kufanya ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba
na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa
kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya
taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu
Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja
zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa
nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya
Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu
Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa
Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki
wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa
Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema
yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja
yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii
kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria
za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu.
Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata
kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile
ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba
na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15
Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba
taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200
wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.
Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili
kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu
kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi,
Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia
n.k.
Ndugu
Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini
tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi
hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza
kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye
wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa
mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA.
Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya
TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia
waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata
watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa
sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi
kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu
huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na
makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi
ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum.
Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na
nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na
Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu
Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa
tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi
ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane
hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za
Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza
kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati
mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye
nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo
ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu
Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani
bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao
ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na
msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili
au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale
wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na
kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi
lao.
Ndugu
Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa
iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na
kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu
ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu
Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka
watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali
maslahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao
au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu
Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya
Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika
Muswada. Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu
sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati
kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar.
Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili
kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili
Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea
kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni
suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano
sidhani kama ni sawa.
Ndugu
Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja
ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama
ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa
Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa
maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi
imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina
sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande
kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum
nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu
sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi
ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina
Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila
wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar
nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara
yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa
nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya
Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo
kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge
Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe
kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge
wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu
Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya
Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum
bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya
Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana
na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono
na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali
inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume
kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya
Tume. Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo
linaloweza kujadiliwa.
Ndugu
Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi
viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati
tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya
hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila
maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua,
naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na
maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya
hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.
-jamiiforum