HALI ya mwanamke aliyepigwa risasi na polisi katika Benki ya CRDB mjini hapa, Violet Lyapa (30) bado ni tete huku taarifa zake zikifanywa kuwa siri kubwa.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Hospitali ya Selian, Violet bado amelazwa
katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) huku hali yake
ikibadilikabadilika.
Pamoja na kwamba tukio hilo limechukua siku zaidi ya tano bado hali ya Violet inafanywa kuwa siri nzito.
Mwanamke
huyo amewekewa ulinzi mkali katika wodi aliyolazwa lakini mmoja wa
wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe,
amesema hali ya majeruhi huyo imekuwa ikibadilika kiasi cha kulazimika
kumpa uangalizi maalum.
Jeshi
la polisi mkoani Arusha limekuwa na kigugumizi kutoa taarifa juu ya tukio
hilo na hatua zipi zimechukuliwa juu ya uhalali wa umiliki wa silaha
iliyotumia kuwatishia polisi baada ya kukuta gari lake limetolewa upepo.
Aidha,
katika hali inayotia shaka kigogo wa ngazi za juu mkoani Arusha amekuwa
akimjulia hali mara kwa mara majeruhi huyo hasa nyakati za usiku na
taarifa zilizoenea zinasema kigogo huyo ana uhusiano wa karibu na
majeruhi huyo.
Pia, baadhi ya ndugu wa majeruhi wamelalamikia kuzuiwa kumuona ndugu yao na kutakiwa kuonesha vitambulisho.