CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo baada ya Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Vicent Remoy, kufariki ghafla jana.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Meya wa Manispaa
hiyo, Jafary Michael (CHADEMA), alisema Remoy ambaye pia alikuwa ni
Diwani wa Kata ya Kiboriloni, zahanati ya Jafary iliyoko katikati ya mji
wa Moshi.
“Ni kweli amefariki, na mimi nimepokea taarifa hiyo dakika
30 zilizopita, na kwa mujibu wa taarifa za awali, ni kwamba alienda
kutizama afya yake hapo zahanati baada ya kuhisi kifua kuwa kizito
wakati akiwa shambani kwake Msalanga,” alisema Michael.
Alisema mara
ya mwisho kuzungumza naye kuhusu ugonjwa ilikuwa ni wakati wamesafiri
kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo
ambako alimwambia kuwa amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa miguu
(gauti).
Mstahiki Meya Michael ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA
Manispaa ya Moshi, alisema chama kimepokea kifo hicho kwa mshituko
mkubwa kutokana na ukweli kwamba Remoy ndiye alikuwa muasisi wa chama
katika Manispaa ya Moshi.
“CHADEMA manispaa tumepokea kwa mshituko
mkubwa kifo cha huyu mzee. Mbali ya kuwa muasisi wa chama, pia alikuwa
kiungo muhimu kama mtu mzima kwa wanasiasa ambao ni vijana bila ya
kujali itikadi za kisiasa,” alisema Michael.
Alisema pia marehemu
alikuwa Diwani wa Kata ya Kiboriloni kwa vipindi vitatu mfululizo
kuanzia mwaka 2000 hadi sasa, huku akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
CHADEMA katika Manispaa ya Moshi.
“Naweza
sema alikuwa ni kiongozi mwandamizi ndani ya CHADEMA, na pia
ameshikilia nafasi ya naibu meya kwa vipindi vyote vitatu. Mara ya
mwisho alichaguliwa kwa kura zote ambazo zilipigwa na madiwani wa
CHADEMA na CCM,” alisema Michael.
Alisema mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC na kwamba hadi sasa
chanzo cha kifo chake hakijafahamika