muhtasari

Home » , , » SERIKALI: TUMEJIPANGA KUKABILIANA NA UGAIDI...

SERIKALI: TUMEJIPANGA KUKABILIANA NA UGAIDI...


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali kupitia polisi inaendelea kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya usalama, ukiwamo ugaidi. 
Akitoa hoja ya kuahirisha Bunge Dodoma jana, Pinda alisema matukio ya hivi karibuni nchini Kenya na kukamatwa kwa watuhumiwa nchini ni ishara kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea nchi yoyote.
 
Pinda alirejea matukio ya kukamatwa kwa vijana 12 waliokuwa wakifanya mazoezi msituni mkoani Mtwara na wale waliokamatwa Wilaya ya Kilindi, Tanga, kuwa ni ushahidi unaotoa wajibu wa kuimarishwa kwa ulinzi na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio hayo.
 
Kila kiongozi wa eneo ajue watu wanaoishi katika himaya yake. Kazi hii itasaidia kuepuka tatizo la wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu,” alisema Pinda.
na kuongeza:
 
Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za mitaa na vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi, kwa kuzingatia sheria ya serikali za mitaa na sheria ndogo zilizotungwa ili kuimarisha usalama katika halmashauri husika”.
 
Alisema Serikali imekuwa ikiwahimiza wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi huku wale wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya watu wengi wanaagizwa kufunga kamera za usalama na kuziunganisha kwenye mtandao wa polisi ambao wanaweza kutoa msaada pale uhalifu unapotokea.
 
Mpango wa BRN
Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali imeanzisha vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita zinazosimamia utekelezaji chini wa Matokeo Makubwa sasa (Big Results Now – BRN) na kwamba mfumo huo utakuwa ukitoa taarifa za utekelezaji za kila wiki na kila mwezi.
 
Alisema katika utekelezaji wa miezi mitatu ya mwanzo yamepatikana matokeo katika sekta ya Kilimo ambako miradi 26 ya umwagiliaji kwa wakulima wadogo imetekelezwa, pia ukarabati wa maghala 26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hususan katika eneo la SAGCOT.
 
Aliitaja sekta nyingine kuwa ni Nishati ya Umeme ambako wateja wapya 27,494 wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwishoni mwa 2013/2014.
 
Vipande vya bomba la gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi wa kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari vimewasili nchini, na uchomeleaji wa bomba hilo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umekamilika kwa Kilomita 124.3. vilevile, Kilomita 447 za njia ya bomba la gesi zimesafishwa,”alisema Pinda.

Katika Sekta ya Elimu alisema shule za msingi 5,916 zilipatiwa mitihani ya marejeo na mazoezi na kwamba mafunzo kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa walimu katika shule 1,325 sawa na asilimia 65 ya lengo la shule 2,048.
 
“Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata majisafi na salama kufikia takribani Milioni 15.9,”alisema Pinda na kuongeza:
 
Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini imewezekana baada ya Wizara ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi”.
 
Bunge limeahirishwa hadi Desemba 3 mwaka huu litakapokutana katika Mkutano wa 14 mjini Dodoma.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger