Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema juzi ameangukia pua baada ya Bunge kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Kadhalika Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana
na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika
kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari,
badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa
Serikali na Jaji Werema ambaye Alhamisi wakati akijibu hoja za wabunge
alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo
haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na
hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
“Sitegemei magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya
taifa. Walio wangu watanikataa na wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa
ajili ya taifa sitamwangukia mtu yeyote miguuni,” alisema Werema, kauli
ambayo iliwachefua wabunge.
Hata hivyo, juzi baada ya Spika kuwahoji wabunge
na kukataa mapendekezo ya Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka
hivyo alisimama na kutaka Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu
hicho.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande
wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina
mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema Werema.
Hata hivyo, Spika alikataa na kusema: “Kama kuna
eneo ambalo tumefanyia utani Serikali ni katika eneo hili, naomba
Serikali mtuletee muswada bungeni siyo porojo za maneno.”
Katika marekebisho hayo, Serikali ilikuwa
ikipendekeza katika sheria hiyo mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa
waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya kuandika habari za
uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi kiasi kisichozidi Sh5 milioni.