“TUNAJUA shangazi anatutesa kwa sababu baba na mama wapo mbali, kama
wangekuwepo hapa tusingeteswa hivi. Tunamuomba baba, tunamuomba mama
kama watasoma habari hii waje watuchukue turudi nyumbani, shangazi
anatutesa sana, wala hatukutegemea,” ndivyo alivyoanza kusema mtoto
Hassan Yusuf (5) ambaye ni mkubwa kwa wenzake, Hussein Yusuf (5) na
Rehema Said (5).
Ikifika mahali mtoto mdogo anasema anawakumbuka wazazi wake kwa
sababu ya mateso anayoyapata ugenini ujue ni zaidi ya ukatili, tena ni
ukatili wa kutisha.
Watoto hao, kwa sasa wanaishi Nzasa ‘A’, Kata ya
Charambe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na ndiko walikopatia
mateso yote.
MAMBO YALIPOANZA KUTIBUKA
Wiki iliyopita, watoto hao waliokolewa
na majirani katika kifungo cha miezi sita ndani huku afya zao zikiwa
zimedhoofu kwa kukosa chakula.
Ilidaiwa kwamba, watoto hao Hassan na Hussein ambao ni mapacha na
Rehema, walifungiwa katika banda la shangazi yao aitwaye Asia Bora
ambalo ujenzi wake haujakamilika. Wamekuwa wakiishi humo kwa kula mabaki
ya vyakula jalalani.
USHUHUDA WA MAJIRANI
Wakizungumza na gazeti la Uwazi hivi karibuni,
majirani wa nyumba hiyo walimweleza mwandishi kuwa watoto hao
wamekuwa wakionekana nje ya nyumba hiyo mara chache sana wakiwa
wanagombania mabaki ya vyakula kwenye jalala.
“Tumekuwa tukiwaona nje mara chache kwenye jalala. Unajua, Asia
(shangazi yao) aliwachukua kwa kaka yake, Kijiji cha Namakongoro Kata ya
Lihimalyao huko Kilwa mkoani Lindi.
“Tukasikia lengo lake aje
kuishi nao kwa vile yeye Mungu hamkujalia kupata watoto. Lakini maisha
hapo kwake yakawa siyo mazuri kwa kipato kwa mama huyo.
Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Ramadhan yeye alikwenda mbele zaidi kwa kusema:
“Hapo awali tulikuwa tukiwaona wakitoka nje na kucheza na watoto wetu
huku wakiwa na afya nzuri. Asia akatueleza kuwa ni watoto wa nduguye,
amewachukua huko kijijini.
“Baada ya muda fulani tukawa hatuwaoni, tulidhani amawarudisha kwao,
lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda mbele tukawa tunawaona mara
chache wakiwa jalalani wanapigania mabaki ya chakula.
“Kuna siku
mimi niliwakamata wakiwa wamebeba mfuko wa rambo wenye kinyesi, walikuwa
wanakuja kutupa katika maeneo yetu, nikawarudisha nao kwa shangazi yao.
Kumbe nyumba wanayoishi haina choo ndiyo maana wamekuwa wakijisaidia
kwenye rambo.
“Siku moja walipotoka nje kutafuta chakula jalalani, mimi na majirani
wenzangu tuliwauliza wanaishije? Wakatuambia hawapewi chakula na
shangazi yao akitoka asubuhi harudi mapema, akirudi inakuwa ni usiku
sana wao wakiwa wameshalala.
“Inasikitisha sana kuwaona watoto hawa wanaachwa peke yao kutwa nzima
bila mtu wa kukaa nao na wamekuwa wakifungiwa ndani kwa muda mrefu
sasa, ila huwa wanakiuka masharti na kutoka kwa ajili ya kutafuta mabaki
ya chakula.
Jirani huyo akaendelea kuanika mateso ya watoto hao: “Kwa kuwaonea
huruma tumekuwa tukilazimika kuwapa chakula, lakini Asia anaporudi na
kugundua hilo anawapiga, kwa hiyo wakawa waoga kuja kuchukua chakula.
Mimi niliumia hadi machozi.”
Jirani: “Baadaye wakawa hawaonekani, lakini cha ajabu mara nyingi
tukiamka asubuhi tunakuta mifuko ya rambo yenye vinyesi imetapakaa,
tukimweleza Asia inakuwa ugomvi.
“Siku moja baada ya shangazi yao
kuondoka, nilikwenda kuwachungulia ndani, nikawaona wamekonda sana,
wamepauka na wamevaa nguo zilizochakaa.
“Nilitokwa machozi, nililazimika kuwaita wenzangu nao walipofika
hakuna aliyejizuia kulia. Tukasema hawa watoto watakufa, ndiyo tukaamua
kuwaokoa kwa kupeleka taarifa kwa mzee Dadi Salum ambaye ni polisi jamii
wa hapa.
POLISI JAMII NAYE ALIA
“Mzee Dadi naye alipofika na kuwaona kwa
macho alilia, watu wakaanza kukusanyika, tukawatoa nje watoto, kila
mmoja aliwaonea huruma. Tuliwachukua hadi Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa
Nzasa A.
SHANGAZI MTU ANUSURUKA KIPIGO
“Hatujui ni nani aliyempigia simu
Asia, kwani muda mfupi tu tukasikia yupo nyumbani kwake. Uongozi wa mtaa
ulimfuata, walipofika, wanawake wenzake hasa wale anaochukua nao mkopo
wa fedha benki walitaka kumpiga wakimuuliza pesa anapeleka wapi.
“Hata hivyo aliokolewa na polisi jamii ambao walimchukua na kumweka
katika Bajaj na kumpeleka Kituo cha Polisi Mbagala kwenye Dawati la
Jinsia na Watoto, watoto nao pia walipelekwa huko.”
Naye Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Nzasa A, Mrisho Salum alikiri kuwapokea watoto
hao wakiwa katika hali mbaya kiafya, wakapelekwa polisi. Akawataka
wananchi kutokaa kimya mara wanapoona vitendo kama hivyo.
Mwandishi alifika hadi kituo cha polisi na kuambiwa na askari mmoja
kuwa mapacha walichukuliwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Othman
Mbwana aliyedai ni babu yao.
Mbwana alidai kwamba ameamua kuwachukua watoto hao wakaishi nyumbani kwake wakati akifanya mawasiliano na wazazi wao.
“Kwanza nitawapeleka hospitali wakatazamwe afya zao, ila
nimesikitishwa sana na hali hii, sijajua ni kwa nini watoto hawa
wamefikia hatua hii,” alisema Mbwana.
Rehema yeye alichukuliwa na
mjomba wake aitwaye Sood Ismail ambaye alidai anakwenda kukaa naye hadi
hapo atakapofanya mawasiliano na wazazi wa huyo mtoto, akisema kitendo
cha Asia kimeidhalilisha familia.
RPC TEMEKE ATUPIA NENO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Engelbert Kiondo amewataka wananchi kufichua vitendo viovu ndani ya
jamii na amewapongeza vijana wake wa ulinzi shirikishi kuokoa maisha ya
hao watoto.
Source: Gazeti la Uwazi/ Global publisher